Wajasiriamali wadogo zaidi ya 450 wanufaika na mafunzo ya OSHA

Zaidi ya wajasiriamali wadogo 450 wamenufaika na mafunzo ya Usalama na Afya kazini ambayo yametolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika mikoa ya kusini hivi karibuni.

Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo wa kuvitambua vihatarishi mbali mbali vinavyotokana na shughuli zao za kila siku na kuvidhibiti ili kujiepusha na ajali pamoja na magonjwa ambayo husababishwa na vihatarishi husika.

Takwimu hizo zimetolewa na Mkaguzi Mwandamizi wa Usalama katika sehemu za kazi wa OSHA, Bw. Sam Sichone, alipokuwa akifanya mahojiano na vyombo vya habari mara baada ya kuhitimisha mada yake katika moja ya darasa la mafunzo kwa wajasiriamali mkoani Lindi.

Mafunzo hayo yanaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya vijana ambayo yamefanyika kitaifa mkoani Lindi.

Bw. Sichone alisema wajasiriamali wadogo wanajishughulisha na kilimo, uvuvi, usindikaji wa vyakula, ufundi, ushonaji na makundi mengineyo katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi ndio wamepatiwa mafunzo hayo.

“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa makundi tajwa kwani watu wengi katika makundi hayo wamekuwa wakifanya kazi hatarishi sana bila kuzingatia kwamba shughuli wanazozifanya huambatana na vihatarishi mbali mbali vya kiusalama na afya ambavyo vinaweza kuwasababishia ajali ama magonjwa,” alieleza Sichone.

Mshirki wa mafunzo, Bi. Asha Hamis, alisema: “Tumejifunza mambo mengi sana kuhusu afya na usalama tunapokuwa kazini hivyo tutakwenda kuboresha mazingira yetu ya kazi ili kujiepusha na magonjwa na ajali.”

 

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *