RC awataka waajiri kutekeleza Sheria ya Afya na Usalama kazini

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, amewaagiza wamiliki wa viwanda kutekeleza ipasavyo Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa kazi yenye lengo la kuwalinda wafanyakazi dhidi vihatarishi mbali mbali ambavyo husababisha magonjwa na ajali katika sehemu za kazi.

Maagizo hayo ameyatoa alipotembelea banda la OSHA kwenye maonesho ya viwanda mkoa wa Pwani ambayo yanafanyika katika viwanja vya ofisi yake Kibaha mkoani Pwani.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Ndikilo amesema kutokana na uwepo wa viwanda vingi katika mkoa wa Pwani ambapo shughuli zake huambatana na vihatarishi mbali mbali vya kiusalama na afya, ni lazima kuweka mkazo katika kulinda afya na usalama wa wafanyakazi.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa OSHA, Bw. Eleuter Mbilinyi, amesema taasisi yake inashiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kutoa ushauri wa kitaalam kwa wenye viwanda kuhusu namna ya kuimarisha mifumo ya kuwalinda wafanyakazi dhidi athari mbali mbali zitokanazo na kazi.

Nae Alex Mosha, ambaye ni mfanyakazi wa TANESCO ameishauri taasisi ya OSHA kutembelea maeneo mbali mbali ya kazi na kuzungumza na wafanyakazi ili kuwaongezea uelewa kuhusu Afya na Usalama wao wanapokuwa kazini.

Maonesho ya viwanda mkoa wa Pwani yalizinduliwa tarehe 17 kwa niaba ya Makamu wa Rais na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya na kufungwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Jumamosi tarehe 19. 

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *