• +255-22-2760548/2760552
 • info@osha.go.tz

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JITIHADA ZA OSHA KATIKA KUWEZESHA UCHUMI WA VIWANDA

TAARIFA KWA UMMA

JITIHADA ZA OSHA KATIKA KUWEZESHA UCHUMI WA VIWANDA NA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI NCHINI.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuwainua watanzania kutoka katika kipato cha chini kwenda kipato cha kati kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo mkazo wake ni kujenga uchumi wa viwanda. Serikali imeendelea kufanya jitihada mbali mbali ili kufikia lengo hilo ambapo miongoni mwa jitahada hizo ni kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kupitia andiko lake (Blue Print) ambalo limeainisha changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi na taasisi mbali mbali ili kufikia azma hiyo.

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), ukiwa ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazohusika moja kwa moja na uwezeshaji wa biashara, unapenda kuwafahamisha wadau wake na umma kwa ujumla kuwa umefanya maboresho mbali mbali katika utoaji wa huduma kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa maazimio yaliyomo kwenye andiko tajwa.

Baadhi ya mambo yaliyoainishwa katika andiko ni pamoja na upunguzaji wa gharama za uendeshaji katika biashara na uwekezaji kwa kupunguza tozo na ada mbalimbali pamoja na kuondoa urasimu katika kutoa huduma ikiwemo kuondoa mwingiliano wa majukumu miongoni mwa taasisi zake. Katika kutekeleza andiko hilo OSHA imefanya mambo yafuatayo;

1. Marekebisho ya sheria kuhusiana na Tozo na Ada.

Wakala umefanya marekebisho ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, 2003 kupitia GN 719 ya Tarehe 16 Novemba 2018 kwa kuondoa tozo mbalimbali kama ifuatavyo;

 • Ada ya Usajili wa eneo la kazi iliyokuwa ikitozwa kati ya Sh. 50,000 hadi Sh.1, 800,000;
 •  Ada ya fomu ya usajili sehemu za kazi iliyokuwa ikitozwa Sh. 2,000;
 •  Faini zinazohusiana na vifaa vya kuzimia moto ya Sh. 500,000 ambayo ilikuwa inaingiliana na taratibu zinazosimamiwa na Jeshi la Zimamoto ya Uokozi.
 •  Ada ya Leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Afya na Usalama iliyokuwa inatozwa Sh 200,000 kwa mwaka; na
 • Tozo ya ushauri wa kitaalamu wa Usalama na Afya ya Sh 450,000 kwa saa kwa mtaalam mmoja.

Matokeo ya kuondoa tozo na ada hizi ni pamoja na ongezeko kubwa la sehemu za kazi ambazo zimesajiliwa. Kwa mfano: kwa mwaka wa fedha 2018/19 sehemu za kazi zipatazo 16,457 zilisajiliwa ukilinganisha na 3,354 zilizosajiliwa kwa mwaka 2017/18 kabla ya kuondoa tozo hizo. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 491(491%). Katika utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003, ongezeko hili linamaanisha kwamba sehemu nyingi za kazi zimefikiwa na OSHA na idadi ya kaguzi zimeongezeka na hivyo hali ya usalama na afya mahali pa kazi inazidi kuimarika nchini.

2. Kuondoa Urasimu

Katika Kuondoa urasimu wa utoaji huduma, Wakala umefanya mapitio ya Mlolongo wa Biashara (Business Process Review) ili kubaini maeneo yanayoleta urasimu katika utekelezaji wa majukumu na katika mapitio hayo OSHA tumefanikiwa kufanya yafuatayo:

 •  Kupunguza muda wa kupata Cheti cha Usajili wa sehemu ya kazi (Registration Certificate) kutoka siku 14 hadi siku 1 baada ya mwombaji kukamilisha mahitaji yote ya usajili.
 •  Kupunguza muda wa kushughulikia na kutoa Leseni ya Kukidhi matakwa ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi (Compliance License) kutoka siku 28 hadi siku 3 baada ya kukamilisha taratibu zote muhimu.

3. Usimikaji wa Mfumo wa Tehama

OSHA ipo katika hatua za mwisho za kusimika mfumo wa TEHEMA ujulikanao kama (Workplace Inspection Management System (WIMS) ambapo kupitia mfumo huo usajili wa maeneo ya kazi utafanyika kwa njia ya kielektroniki hivyo kusogeza huduma zaidi na kupunguza mlolongo wa kupata cheti na huduma zingine za kaguzi. Aidha, mfumo huu utakuwa na uwezo wa kuunganishwa na mifumo mingine ndani ya serikali, hivyo kurahisisha upatikaji wa taarifa.

4. Kuongeza Uwajibikaji

Wakala umeongeza uwajibikaji na kuimarisha mifumo ya usimamizi. Hii ni pamoja na kuanzisha dawati la kushughulikia kero na malalamiko mbali mbali ya wadau. OSHA imeanzisha pia utaratibu wa wakaguzi wake kufanya kaguzi kwa timu badala ya mkaguzi mmoja mmoja. Utaratibu huu unalenga kuongeza uwazi katika ukaguzi na hivyo kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji huduma na kuondoa usumbufu kwenye maeneo ya kazi kwa kila mkaguzi kuingia eneo la kazi kwa wakati wake. Utaratibu huu umesaidia sana kupunguza malalamiko na kuongeza ufanisi.

5. Uratibu wa Ukaguzi kupitia Makao Makuu ya taasisi/kampuni (Corporate Inspections)

Wakala umeendelea kuwahamasisha wafanya biashara, makampuni ama wawekezaji wenye ofisi na matawi mengi katika mikoa mbalimbali nchini

kuratibu shughuli za ukaguzi, mafunzo na upimaji afya kwa kupitia ofisi zao za Makao Makuu ili;

 • Ziweze kufanyiwa ukaguzi, mafunzo na upimaji afya kwa wakati mmoja badala ya kila ofisi kufanya ukaguzi kwa wakati wake.
 • Kurahisisha upatikanaji wa Leseni ya kukidhi matakwa ya usalama mahali pa kazi kwa ambayo hutolewa kwa ofisi na matawi yote nchini kwa wakati mwafaka.
 • Kuwarahisishia waajiri kupanga ratiba ya ukaguzi na masuala ya kibajeti yanayohusu Usalama na Afya katika sehemu zao za kazi.
 • Kuwezesha menejimenti kupata mrejesho wa hali ya Usalama na Afya katika maeneo yao yote nchini kwa wakati kwaajili ya utekelezaji kwa mujibu wa Sheria.

6. Kuongeza uelewa wa masuala ya Usalama na Afya miongoni mwa wadau hususani katika sekta isiyo rasmi.

Katika kipindi cha hivi karibuni, serikali kupitia OSHA imekuwa ikigharamia mafunzo kwa wenye viwanda vidogo, wajasiriamali wadogo na vikundi vya walemavu wanaojishughulisha na usindikaji wa vyakula, ushonaji na utengenezaji batiki, wachimbaji wadogo, mafundi, wakulima, wanaofanya usafi wa barabara na sehemu nyingine zinazotumiwa na umma. Jumla ya wajasiriamali wadogo 28,275 walinufaika na programu hii ya mafunzo katika mikoa ya Tabora, Mtwara, Ruvuma, Dodoma, Arusha, Mbeya, Mwanza, Iringa, Shinyanga, Pwani, Songwe, Singida, Kilimanjaro, Rukwa na Dar Es Salaam. Matokeo ya programu hii ambayo ni endelevu, yalipelekea kupata uelewa wa namna ya kujikinga na vihatarishi vinavyoendana na shughuli zao za kiuchumi.

Hivyo, mafunzo haya na mengine wanayoyapata husadia kuwahamasisha kujua umuhimu wa kurasimisha biashara zao bila kuwa na hofu ya tozo na ada kwani wanatambua kuwa afya na usalama wao ndio rasilimali kubwa katika uzalishaji. Programu hizi ni muhimu hasa kwa kuzingatia kuwa sekta isiyo rasmi inaajiri watu wengi na ndio yenye mazingira hatarishi zaidi kwa kukosekana mifumo rasmi ya usimamizi.

7. Kuimarisha ushirikiano na Taasisi nyingine za umma na binafsi.

Miongoni mwa changamoto zilizoainishwa katika Andiko la Blueprint ni pamoja na mwingiliano wa majukumu ya OSHA na taasisi nyingine kama TBS, TFDA, ERB n.k. Katika kushughulika changamoto hii, OSHA inafanya yafuatayo;

 •  Kushirikiana na taasisi nyingine za serikali kama vile Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ( WCF), Shirika na Viwango la Taifa (TBS); katika kuandaa viwango, Mkemia Mkuu wa Serikali katika kubadilishana taarifa, ERB na CRB; katika kutambua miradi ya ujenzi inayoanzishwa nchini pamoja na NBS,BRELA;TRA katika kupata taarifa za maeneo ya kazi nchini.
 • Kushiriki katika kutoa elimu ya masuala ya Usalama na Afya kwa wadau katika sekta ya umma na makampuni binafsi.
 •  Kushirikiana na taasisi nyingine ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu (OWM- KVA) kufanya kaguzi za pamoja kama vile Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Idara ya Kazi, NSSF, PSSSF na nyinginezo.
 • Kushiriki kikamilifu katika kutoa huduma katika dawati la pamoja lililopo chini ya Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania (TIC).
 • OSHA inashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na taasisi nyingine katika programu ya Kliniki ya Biashara (Business Clinic) inayoratibiwa na Mamlaka ya Uendelezaji Biashara ya Tanzania (TANTRADE).

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA); ni taasisi ya umma yenye dhamana ya kulinda Usalama na Afya wa wafanyakazi wanapokuwa katika sehemu zao za kazi kupitia usimamizi wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Majukumu ya msingi yanayotekelezwa na OSHA chini ya Sheria tajwa ni pamoja na; Kufanya ukaguzi wa Usalama na Afya katika sehemu za kazi,

kupima afya za wafanyakazi kulingana na kazi wanazofanya, kutoa mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa kazi, kuchunguza ajali zinazotokea katika sehemu za kazi pamoja na kuishauri serikali katika utungaji wa Sheria, Sera, Kanuni, Miongozo na Mikataba ya Kimataifa inayohusu usimamizi wa Usalama na Afya katika sehemu za kazi.

Hivyo, tunawakumbusha wadau wetu na umma kwa ujumla kuendelea kuzingatia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, 2003 kwa kusajili maeneo yao ya kazi na kuhakikisha kwamba yamefanyiwa ukaguzi ili kukidhi matakwa ya Sheria na kuboresha usalama na afya katika sehemu za kazi.

Usalama na Afya kazini kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda

Kwa taarifa zaidi;

Tembelea tovuti yetu (www.osha.go.tz);

Tupigie kupitia simu ya bure: 0800110091/0800110092 au;

Tutumie barua pepe kupitia: info@osha.go.tz.

IMETOLEWA NA;

KAIMU MTENDAJI MKUU

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI (OSHA)