• +255-22-2760548/2760552
 • info@osha.go.tz

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

Haki na Majukumu ya Mwajiri

TAFSIRI

Mtu yeyote anaeajiri au kumpa kazi mtu mwingine na kumlipa mshahara/ujira kwa kazi hiyo anaitwa mwajiri kwa mujibu wa Sheria ya Afya na Usalama Mahala pa Kazi ya mwaka 2003.

HAKI NA MAJUKUMU

Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 imeweka bayana majukumu ya mwajiri kuhusiana na usalama na afya mahala pa kazi.  Hata hivyo, majukumu yafuatayo ni muhimu kuzingatiwa: 

Majukumu ya jumla:

 1. Kuhakikisha mahala pa kazi ni salama na kuwalinda wafanyakazi dhidi ya ajali, majeraha na madhara ya kiafya yanayoweza kuzuilika. Hii ni pamoja na kufanya mabadiliko katika muundo, michakato na mazingira ya kazi, kama vile, kupunguza kiwango cha kemikali na vihatarishi vingine vinavyoweza kuwaathiri wafanyakazi, kufuatilia madhara yatokanayo na vitu hivyo na kuweka kumbukumbu.  
 2. Kuanzisha, kupitia na kuwasilisha taratibu za kazi kwa wafanyakazi ili wafuate mahitaji ya usalama na afya.
 3. Kuwapatia wafanyakazi wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi ulinzi wa kutosha na vifaa kinga vinavyohitajika. Hii ni pamoja na kutoa vifaa kinga kama vile vifunika uso, glovu na vifaa kinga dhidi ya kelele; kutumia kemikali ambazo hazina madhara makubwa kiafya; au kuboresha mzunguko wa hewa safi.
 4. Kuhakikisha usalama wa mazingira ya kazi kwa wafanyakazi na watu wengine wanaotembelea mahala pa kazi.  

Majukumu Maalum/Mahsusi:

 1. Kubandika mabango, lebo na maelekezo yenye alama na/au taratibu zilizo rahisi kueleweka kuhusu namna ya kuzuia na kushughulikia ajali na majeraha au dharura mahala pa kazi baada ya tukio.
 2. Kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanatumia vifaa vilivyo salama na kuvifanyia matengenezo vifaa hivyo.
 3. Kutoa mafunzo ya usalama kwa wafanyakazi kuhusu mbinu mahsusi za kuhakikisha usalama na afya katika lugha ambayo wanaielewa.
 4. Kufanya vipimo na uchunguzi wa afya wa wafanyakazi kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi kwa ajili ya kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa katika hali inayowawezesha kufanya kazi na kutunza afya na ustawi wao.
 5. Kuruhusu wafanyakazi au wawakilishi wao walioidhinishwa waweze kuona kumbukumbu za tiba na zinazohusu mazingira ya hatari ambayo wamekuwemo.
 6. Kuweka kumbukumbu sahihi zinazohusu majeraha na magonjwa yanayotokana na kazi.
 7. Kutoa taarifa OSHA kuhusu ajali au magonjwa yanayotokea katika maeneo ya kazi.
 8. Kusaidia wafanyakazi watumie haki yao ya kutoa taarifa kuhusu majeraha, ugonjwa au kifo vinavyotokana na kazi.

Mambo ya kuzingatia kukidhi viwango vya Usalama na Afya katika eneo la Kazi

Ni lazima waajiri wote wafuate na kukidhi masharti na viwango vya OSHA vinavyohusu aina ya shughuli wanazozifanya. Mhusika mkuu mahala pa kazi ni Meneja Rasilimali watu au Afisa Usalama. Afisa Usalama anahusika zaidi katika sekta hatarishi zikiwemo sekta ya uzalishaji, ujenzi, madini na usafirishaji. Kuwa na orodha maalum yenye vipengele muhimu vya kuzingatia inaweza kuwasaidia waajiri na mameneja Rasilimali watu/maafisa usalama kupima kama wamekidhi masharti yote ya OSHA. Orodha hii inajumuisha mambo yafuatayo:

 1. Sajili sehemu yako ya kazi na upatiwe cheti za usajili
 2. Fanya tathmini ya vihatarishi vya kiusalama na kiafya katika eneo lako la kazi walau kila mwaka
 3. Andaa sera ya Usalama na Afya katika sehemu yako ya kazi
 4. Hakikisha kwamba kaguzi zote za kiusalama na kiafya zilizopo kwa mujibu wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 zimefanywa na Wakaguzi wanaotambulika na serikali katika eneo lako la kazi
 5. Hakikisha kwamba wafanyakazi wako wanakuwa na afya njema kwa kuwapima afya zao
 6. Hakikisha kwamba wafanyakazi wako wamepatiwa mafunzo ya Huduma ya Kwanza na ya kamati za Afya na Usalama

Mwongozo zaidi wa namna ya kutekeleza matakwa haya ya kisheria, mwajiri atayapata wakati wa kufanya usajili wa sehemu yake ya kazi ama kwa kuwasilisha maombi yake ya kupatiwa msaada zaidi kupitia njia mbali mbali za mawasiliano ikiwemo kupiga simu zetu za bure (0800110091/0800110092).

Aidha, wasimamizi wa usalama na afya katika sehemu za kazi wanapaswa kuzingatia kwamba maeneo muhimu ambayo Wakaguzi wa Usalama na Afya wa OSHA wanaangalia wakati wa ukaguzi ni pamoja na:

 1. Hatari zinazoweza kutokea
 2. vifo na majanga
 3. malalamiko ya wafanyakazi/majirani rufaa
 4. ufuatiliaji na kaguzi zilizopangwa.

Ukaguzi wa OSHA huanza kwa kikao cha pamoja na menejimenti ya eneo husika kwa ajili ya kufahamiana na kufahamishana kuhusu ukaguzi unaotarajiwa kufanyika na baada ya ukaguzi kukamilika, wakaguzi wa OSHA huhitimisha kazi yao kwa kufanya kikao ambapo menejimenti hupewa taarifa ya awali ya ukaguzi uliofanyika na hatua zinazopaswa kuchukuliwa baada ya hapo. 

 

Dhima

Kuhakikisha usalama na afya ya wafanyakazi Tanzania Bara kwa kudhibiti, kusimamia utekelezaji, na kuendeleza viwango imara vya Usalama na Afya kazini kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Dira

Kuhakikisha sehemu za kazi ni salama na zenye Afya