Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

Ujumbe wa mtendaji mkuu

UJUMBE WA MTENDAJI MKUU

Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) ni chombo cha kusimamia usalama na afya mahala pa kazi kwa kuhakikisha kwamba waajiri wote nchini wanaweka miundo na mifumo inayohakikisha usalama na afya mahala pa kazi vinalindwa.  

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la idadi ya waajiri wanaotuma maombi kuomba kukaguliwa au mafunzo ya usalama na afya makazini mwao. Hiki ni kiashiria muhimu cha mafanikio. Taasisi ya OSHA inatia mkazo katika kuelimisha kuliko kuadhibu ili kuhakikisha kwamba waajiri wanawajibika bila shurti.  

Hata hivyo, bado tunakabiliwa na changamoto kuu mbili; i) uelewa mdogo miongoni mwa waajiri na wafanyakazi kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya usalama na afya kazini, na ii) ukiukwaji wa masharti kwa kutozingatia viwango vya usalama na afya. Changamoto ya pili inatokana na imani isiyo sahihi miongoni mwa baadhi ya waajiri kwamba gharama za kuhakikisha usalama na afya mahala pa kazi ni kubwa sana, tofauti na hali halisi inavyoonesha. Utafiti umethibitisha kwamba faida zitokanazo na mazingira ya usalama na afya mahala pa kazi ni kubwa kuliko gharama. 

Kama Mkurugenzi wa taasisi hii nyeti, maono yangu kwa miaka mitano ijayo ni haya yafuatayo:

1) Kwamba OSHA inatilia mkazo suala la kuongeza tija kwa kusimamia viwango vya usalama na kulinda afya ya mfanyakazi anapokuwa kazini ili kuongeza tija. Ajali, madhara ya kiafya na vifo vinavyotokana na shughuli za kazi vikipungua, tija inaongezeka.

2) Kwamba OSHA inaanzisha mifumo shirikishi kati ya waajiri na taasisi ili kuhakikisha utekelezaji wa hiari wa masharti ya usalama na afya makazini;

3) Kwamba OSHA inatia mkazo uingizaji wa sekta isiyo rasmi yenye wafanyakazi walioajiriwa na waliojiajiri wenyewe katika masuala ya usalama na afya kazini, kwa kubuni mikakati na kuandaa programu maalum endelevu zitakazolinda usalama na afya ya wafanyakazi katika shughuli zote za sekta hiyo;

4) Kwamba OSHA inachangia katika kuongeza ajira zenye staha kama ilivyoainishwa katika malengo ya milenia, hususan lengo Na. 8.

OSHA inaongozwa na ajenda ya ‘Vission Zero’ ambayo baada ya miaka michache ijayo, HAKUNA majeraha na ajali sehemu za kazi; HAKUNA madhara na magonjwa yatokanayo na mazingira ya kazi; na HAKUNA vifo vinavyotokana na kazi.  Tunataka waajiri na wafanyakazi waelewe uhusiano kati ya usalama na afya mahala pa kazi na kuongezeka kwa tija na uzalishaji; waajiri wanatambua kwamba gharama za kuhakikisha usalama na afya mahala pa kazi hazifikii ukubwa wa faida zinazopatikana; na wafanyakazi wanaona umuhimu wa kutumia vifaa kinga wanapokuwa kazini na/au kudai vifaa hivyo kwa waajiri wao pale ambapo havitolewi.   

Tukifanikisha hilo, tutachangia kuongezeka kwa pato la taifa kwa kuongeza tija na uzalishaji mahala pa kazi, na kuondoa mzunguko wa umaskini usio na mwisho kwa kupunguza au kutokomeza kabisa ajali, maradhi, ulemavu na vifo mahala pa kazi. Tutaendelea kuelimisha waajiri na wafanyakazi kuhusu uhusiano uliopo katika ya usalama na afya mahala pa kazi, kuongezeka kwa tija na uzalishaji, kukua kwa pato la taifa, na uwezo wa Serikali kutoa huduma bora za jamii.