Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

Kuelekea siku ya Usalama na Afya Duniani Serikali yawaalika wadau Mkoani Morogoro

Kuelekea siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani, Serikali imetoa wito kwa waajiri na wafanyakazi kushiriki kikamilifu katika kampeni ya maadhimisho hayo inayojumuisha shughuli mbali mbali zikiwemo maonesho, shindano la tuzo na mafunzo ya usalama na afya kwa makundi mbali mbali.

Akizungumza katika mkutano wa Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho hayo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amesema maandalizi ya maadhimisho hayo ambayo yatafanyika Kitaifa Mkoani Morogoro yamekamilika.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau wetu wa utatu tunaendesha kampeni maalum ya kuhamaisha uwepo wa mazingira salama ya kufanyia kazi kupitia shughuli mbali yakiwemo maonesho ya usalama na afya mahali pa kazi, mafunzo ya usalama na afya kwa wafanyakazi wa viwandani, wajasiriamali wadogo, wachimabaji madini na watu wenye ulemavu,” ameeleza Waziri.

Shughuli nyingine zilizoainishwa katika kampeni hiyo na Waziri Ndalichako ni pamoja na shindano la tuzo kwa maeneo ya kazi yanayozingatia ipasavyo viwango vya usalama na afya mahali pa kazi pamoja na kuwahamasisha waajiri na wafanyakazi kujumuika pamoja katika siku ya kilele ili kutafakari hali ya usalama na afya nchini pamoja na kuwakumbuka wafanyakazi walioumia ama kupoteza maisha wakiwa wanatekeleza majukumu yao.

“Napenda kutumia fursa hii kuwaalika wamiliki wa sehemu za kazi, waajiri, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika shughuli zote zinazohusu maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi zilizoainishwa ambazo zinafanyika katika Uwanja wa Tumbaku Mkoani Morogoro,” amesema Prof. Ndalichako.

Kwa mujibu wa Waziri Prof. Ndalichako, inatarajiwa kwamba kampeni ya maadhimisho ya mwaka huu itasaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza uelewa wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi miongoni mwa Watanzania wote na hivyo kuongeza ari ya kuzingatia taratibu muhimu za usalama na afya katika shughuli zao za kila siku.

Akimkaribisha Waziri katika Mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema kupitia maadhimisho hayo Taasisi yake itaendelea kutekeleza programu Atamizi ya Wajasiriamali wadogo ambao watapatiwa mafunzo pamoja na kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na wenzao kuhusiana na mifumo ya usalama na afya kwenye maeneo ya kazi.

Kwa upande wao wadau wa utatu katika usimamizi wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi wakiwemo Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA),  Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri (ATE), Bi. Suzanne Ndomba-Doran na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bi. Getrude Sima, wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kusimamia Usalama na Afya kazini hapa nchini.

"Tunaipongeza sana Serikali ya Tanzania kwanza kwakuwa na Taasisi mahsusi ya kusimamia Usalama na Afya ambayo pia inafanya kazi nzuri kwa kiwango cha kuzivutia nchi mbali mbali kuja nchini kujifunza hivyo tunawashauri waendelee kuweka jitihada zaidi na ikibidi serikali iweze kuridhia mikataba ya Kimataifa ambayo bado haijaridhiwa," amesema Bi Getrude Sima, alipokuwa anatoa salamu za ILO.