Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

OSHA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR KUSHIRIKIANA KUIMARISHA USALAMA NA AFYA KAZINI

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na Idara ya Usalama na Afya Kazini ya Zanzibar wamesaini makubaliano ya mashirikiano katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya baina ya pande hizo mbili.

Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika leo mjini Zanzibar na kushuhudiwa na Waziri katika Afisi ya Rais-Kazi, Uchumi na Uwekezaji ya Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu wa katika Afisi ya Rais-Kazi, Uchumi na Uwekezaji ya Zanzibar, Bi. Maryam Juma Abdulla, Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu na Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Meru.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Soraga amesema makubaliano hayo yatakuwa na nafasi muhimu katika kukuza mashirikiano yaliyokuwepo tangu zamani katika ya OSHA Bara na Zanzibar.

Kwa mujibu wa Mtendaji wa OSHA mkataba wa makubaliano uliosainiwa leo unahusisha ushirikiano katika maeneo makuu matatu yakiwemo kushirikiana katika kuwajengea uwezo watumishi wa pande zote mbili, kuimarisha usimamizi wa Sheria zinazohusu Usalama na Afya pamoja na kuratibu masuala ya Usalama na Afya kwa pamoja.

“Bila shaka mchakato wa makubaliano haya umeshirikisha kikamilifu wataalam wa pande zote mbili na umezingatia matakwa muhimu yaliyopo katika Sheria Na. 8 ya Usalama na Afya ya Zanzibar ya mwaka 2005 pamoja na Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya mahali pa kazi ya mwaka 2003 ya Tanzania Bara pamoja na maslahi mapana wadau wetu muhimu.

Aidha, ametoa wito wa kwa viongozi wa Taasisi za umma na binafsi kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mifumo ya usalama na afya kwenye maeneo ya kazi pamoja na kutenga rasilimali zote muhimu zinazohitajika katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya kazini.

Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Jamal Katundu, amesema makubaliano hayo ni zao la maelekezo ya viongozi wa juu ambao wamekuwa wakizitaka Wizara na Taasisi zisizo za kimuungano kuangalia uwezekano wa kushirikiana katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Mheshimiwa Waziri nikuhakikishie kwamba mimi na Katibu Mkuu mwenzangu Bi. Maryam tutakuwa tayari kusimamia utekelezaji wa makubaliano haya ambayo OSHA na Idara ya Usalama na Afya ya Zanzibar wameingia leo na hivyo kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa,” ameeleza Prof. Katundu.

Kwa upande wao, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda na Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Afya, Dkt. Ali Said Nyanga wameeleza kufurahishwa kwao na hatua hiyo muhimu ya kuingia makubaliano jambo ambalo wanaamini litakuwa na manufaa kwa pande zote mbili.

“Ninawashukuru viongozi wa Idara ya Usalama na Afya kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na OSHA kwa upande wa Tanzania Bara katika kusimamia ustawi wa wafanyakazi jambo lililopelekea wao kuja kwetu kujifunza kwa ajili ya kuweza kuchukua yale mazuri yanayoweza kusaidia katika kuleta ustawi wa wafanyakazi kwa hapa Zanzibar,” ameeleza Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA. 

“Makubalinao haya tunayoingia leo ni moja ya jitihada tunazozichukua katika kushughulikia changamoto mbali mbali katika usimamizi wa taratibu za usalama na afya ikiwemo upungufu wa watumishi na rasilimali nyinginezo. Kupitia mashirikiano haya tunakwenda kuimarisha zaidi usimamizi wa viwango vya usalama na afya kwenye maeneo ya kazi na hivyo kuhakikisha kwamba usalama na afya unaimarika katika maeneo ya kazi,” amesema Dkt. Nyanga.

Zoezi la utiaji saini makubaliano husika lilitanguliwa na siku mbili za ukaguzi wa mifumo ya Usalama na Afya katika Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Afisi ya Rais-Kazi, Uchumi na Uwekezaji, uchunguzi wa afya za wafanyakazi pamoja mafunzo ya kukuza uelewa wa masuala ya usalama na afya kazini miongoni mwa watumishi wa Ofisi husika.