Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

WAZIRI MKUU AKABIDHI OSHA, IDARA YA KAZI MAGARI NA VIFAA VYA BILIONI 4.3


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekabidhi vifaa vya ukaguzi na magari 30 kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na Idara ya Kazi vilivyonunuliwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha utendaji wa Idara hizo za serikali zenye jukumu la kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vya magonjwa na ajali pamoja na kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini.

Amekabidhi vifaa hivyo katika hafla maalum iliyofanyika katika viwanja vya Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mtumba Jijini Dodoma leo (Agosti 7, 2023).

Vifaa vilivyokabidhiwa ambavyo thamani yake ni bilioni 4.3 ni pamoja na mashine zinazotumika kuchunguza afya za wafanyakazi ikiwemo mashine ya kupima macho ya VT1 Master, mashine ya kupima masikio, mashine ya kuchunguza mapafu, vifaa vya kupima usalama wa umeme pamoja na magari 13 kwa Taasisi ya OSHA na mengine 17 kwa Ofisi za Mikoa za Idara ya Kazi ambazo zipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).  

Akiwasilisha hotuba yake katika hafla hiyo, Waziri Mkuu amewataka watumishi katika Taasisi na Idara zilizokabidhiwa magari na vifaa tajwa kuongeza juhudi na kuzingatia weledi katika utekelezaji majukumu yao ya msingi ili vifaa walivyopatiwa na serikali viweze kuleta tija inayokusudiwa.

“Ninawaagiza Taasisi na Idara zinazopokea magari na vifaa hivi leo kuvitunza na kuhakikisha kwamba vinatumika katika shughuli za kiofisi pekee. Magari haya wakabidhiwe madereva wenye weledi na yatumike kuwafikia wananchi walioko katika maeneo ya pembezoni,” ameagizi Kiongozi huyo Mkuu wa shughuli za Serikali.

Maagizo mengine aliyoyatoa ni pamoja na OSHA na Idara ya Kazi kuhakikisha kwamba wanaongeza idadi ya kaguzi katika maeneo ya kazi, kutenga muda kutatua kero za wananchi na kutatua changamoto zao katika ngazi ya chini kabla changamoto hizo hazijawafikia viongozi wa juu, kukarabati magari yaliyoharibika pamoja na kuyauza au kuwakopesha watumishi magari ambayo hayaweze kutumika tena serikalini.

Aidha, Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali itanunua magari mengine 20 kwa ajili ya Taasisi ya OSHA pamoja na mengine nane (8) kwa ajili ya Idara ya Kazi ili kuendelea kuimarisha uwezo wa Taasisi hizo kuwahudumia Watanzania.

Awali, wakati akimkaribisha Waziri Mkuu katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako alieleza majukumu ya msingi ya Taasisi ya OSHA kuwa na kulinda nguvukazi ya Taifa pamoja na mitaji ya wawekezaji kupitia kutoa ushauri wa kitaalaam na miongozo inayowezesha kudhibiti ajali, magonjwa, vifo pamoja na uharibifu wa mali mahali pa kazi.

Kadhalika, alieleza upungufu wa magari na vifaa uliokuwa unazikabili Taasisi ya OSHA na Idara ya Kazi ambapo amesema magari na vifaa walivyokabidhiwa na Waziri Mkuu vitasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza changamoto iliyokuwepo na kuziongezea ufanisi OSHA na Idara ya Kazi.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, ameishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa Taasisi ya OSHA katika kuwahudumia Watanzania na hivyo kuiwezesha kwa kuipatia magari, vifaa vya ukaguzi pamoja na kuiongezea idada ya watumishi wapatao 18.

Kwa upande wao wadau wa utatu katika masuala ya usalama na afya kazini ambao ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wameipongeza Serikali kwa kuwajali wafanyakazi nchini kupitia uboreshaji wa mazingira ya kazi.

“Tunaipongeza Serikali kwa kushughulikia ombi letu la kuiwezesha OSHA na Idara ya Kazi kutekeleza majukumu yao ipasavyo ambalo tulimfikishia Msheshimiwa Rais siku ya Mei Mosi mwaka huu Mkoani Morogoro kupitia hotuba yetu,” ameeleza Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya alipotoa salamu za wafanyakazi katika hafla hiyo.

“Sisi waajiri tunaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kwamba afya na usalama kazini unaendelea kuimarika katika maeneo yetu ya kazi,” amesema Leonard Selestine ambaye alimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran.