Kamati ya Bunge yaipongeza Serikali kwa mazingira mazuri ya uwekezaji
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza serikali kwa kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini ikiwemo kuhakikisha kwamba kunakuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.
Pongezi hizo zimetolewa na Kamati hiyo ilipofanya ziara katika viwanda vya Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa lengo la kufuatilia uzingatiaji wa taratibu muhimu za usalama na afya kazini miongoni mwa waajiri nchini.
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara katika viwanda vya Bakharesa Flour Mill kilichopo Buguruni na kiwanda cha bidhaa za chuma cha Lodhia Steel Industries Ltd cha Mkuranga Mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Hassan Toufiq ameipongeza serikali kwa kuwawezesha wawekezaji nchini kuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija.
“Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yetu ya kawaida na tumefurahi kuona wenye viwanda tuliowatembelea leo wamepata mafanikio makubwa katika shughuli zao kwani wanafanya uzalishaji mkubwa wa bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi yetu. Wawekezaji hawa wamekiri kupata ushirikiano mkubwa kutoka serikalini ikiwemo Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ambao wamekuwa wakiwasaidia katika kuweka mifumo ya kudhibiti ajali na magonjwa pamoja na kufanya ukaguzi wa mifumo ya umeme na mitambo ya uzalishaji jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa ufanisi wa mitambo husika pamoja na kuiweka katika hali ya usalama wakati wote,” amesema Mwenyekiti Fatma Toufiq.
Aidha, Toufiq amesisitiza kuwa uwekezaji katika viwanda ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya nchi kutokana na faida zake zikiwemo kuzalishaji ajira nyingi, kuongeza upatikanaji wa bidhaa muhimu pamoja na kuongeza pato la Taifa kupitia ulipaji wa kodi.
“Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hasa kwa wawekezaji wa ndani. Tunaishauri serikali kuendelea kujenga mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ili wawekezaji wetu wazidi kukua na kuongeza mtandao wa uzalishaji wao ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu,” amesema Toufiq.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Boniface Mwita, amesema uwekezaji nchini kwa kiwango kikubwa bado unategemea nguvukazi zaidi hivyo ni muhimu kuwekeza katika mifumo ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi.
Awali, wakurugenzi wa viwanda vilivyotembelewa (Bw. Hussein Sufiani-Mkurugenzi wa Mahusiano wa Bakharesa Flour Mill na Sailesh Pandit-Mkurugenzi wa Lodhia Steel Industries Ltd) waliieleza Kamati jinsi walivyoweza kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza uzalishaji kutokana na ushauri ambao umekuwa ukitolewa na wataalam wa OSHA wanapofanya ukaguzi wa usalama na afya katika maeneo yao kila mwaka.
Kwa upande wake Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Jamal Katundu amesema: “Kwa kuzingatia wajibu wa Wizara ya Kazi na Taasisi chini yake ambao ni kusimamia uwepo wa mazingira mazuri ya kazi na kuhakikisha kwamba viwango vya kazi vinazingatiwa, tutaendelea kutekeleza wajibu huo ipasavyo kama tulivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani. Hivyo, niwasihi wawekezaji kuendela kutekeleza taratibu mbali mbali za kazi ikiwemo kuhakikisha kwamba wanalinda afya na usalama wa wafanyakazi.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amewashukuru wawekezaji kwa kutambua mchango wa OSHA katika kukuza biashara zao na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuboresha mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi.
“Tunawaomba wadau wetu waendelee kututumia ili kwa pamoja tuweze kulinda afya za wafanyakazi na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji kwani hakuna jambo lenye thamani zaidi ya uhai wa binadamu. Kazi ni uhai, kazi ni staha kwahiyo lazima tusimamie uwepo wa kazi zenye staha kwani pamoja na kwamba usalama na afya ni suala la kisheria lakini masuala ya usalama na afya ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA.