Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

DANIEL SILLO: OSHA NI WADAU WAKUBWA KATIKA KUKUZA UCHUMI WA NCHI YETU

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Baran Sillo amesema kuwa taasisi ya OSHA ni mdau mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi kwa sababu wanalinda nguvu kazi ya taifa kwa kuhakikisha maeneo ya kazi yanakuwa salama dhidi ya vihararishi vya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Mhe. Sillo ametoa kauli hiyo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikihitimisha ziara ya kutembelea viwanda Mkoani Arusha na Kilimanjaro kwa lengo la kujionea utekelezaji wa sheria na miongozo mbalimbali ya usalama na afya mahali pa kazi katika viwanda hivyo wakiambatana na Naibu wa Waziri - Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi, Katibu Mkuu na watumishi wa Ofisi hiyo pamoja na Wakaguzi wa OSHA.

“OSHA ni wadau wakubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi hii kwa sababu wanalinda nguvu kazi ya taifa ambayo ndio inazalisha hivyo wawekezaji hawa wanapokuwa na nguvu kazi inayozalisha faida inakuja kwa serikali, muwekezaji na kwa wananchi pia kwahiyo niwapongeze sana OSHA kwa kazi hii kubwa mnayoifanya na sisi kamati ya bajeti ambayo jukumu letu kubwa ni kuishauri serikali nasi tutaishauri serikali ili taasisi hii ya OSHA iendelee kuyafikia maeneo ya kazi mengi zaidi nchini ili nguvu kazi hii iendelee kuwa salama na yenye afya na iendelee kuzalisha na kukuza uchumi wa taifa letu” alisema Mhe. Daniel Sillo.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Patrobas Katambi ametoa rai kwa wamiliki wa maeneo ya kazi nchini kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa taasisi ya OSHA kwa sababu taasisi hiyo ipo kwaajili ya kulinda usalama na afya za wafanyakazi pamoja na maeneo yao ya kazi.

“Nguvu kazi ya taifa letu tusipo ilinda athari zake hata uchumi wetu utashuka kwasababu tutakosa wataalam na nguvu kazi itakuwa tegemezi kwa taifa na ndio maana taasisi ya OSHA inafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha maeneo ya kazi yote yanakuwa salama dhidi ya vihatarishi vya ajali na magonjwa, nitoe wito kwa wamiliki wa maeneo yote ya kazi, kuwachukulia OSHA kama marafiki pindi wanapofika katika maeneo ya kazi kwaajili ya shughuli zao za ukaguzi” alisema Mhe. Katambi.

Aidha Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema kuwa taasisi ya OSHA imekuwa ikipokea shuhuda mbalimbali kutoka kwa wamiliki wa maeneo ya kazi wakikiri kuwa kaguzi za usalama na afya pamoja na ushauri wa kitaalamu unaotolewa na OSHA vimesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ushindani wa bidhaa wanazozalisha katika masoko ya kimataifa.

“Wawekezaji wamekuwa wakikiri kwamba ukaguzi wa usalama na afya tunaoufanya pamoja na ushauri wa kitalaam tunaowapatia wawekezaji hawa vimewaongezea tija hususan katika kushindanisha bidhaa zao katika masoko ya kimataifa kwasababu ili uweze kushindana na masoko ya nje ni lazima ukidhi matakwa ya sheria za ndani ikiwemo Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003” alisema Bi. Khadija Mwenda.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilimanjaro Plantation Limited, Bw. Calton Rabenold ambayo ni miongoni wa eneo ya kazi lililotembelewa na Kamati hiyo ameishukuru serikali kupitia taasisi ya OSHA kwa kuendelea kuboresha mifumo ya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.

“OSHA imetusaidia sana kuboresha mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi katika kampuni yetu kupiti kaguzi, mafunzo pamoja na ushauri wanaotoa baada ya kubaini mapungufu na changamoto mbalimbali za kiusalama kupitia kaguzi wanazozifanya na sisi tumekuwa tukifanya maboresho kila tunaposhauriwa “ alisema Bw. Calton Rabenold. 

Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameishukuru sana Kamati hiyo ya Bajeti kwa kufanya ziara ya kutembelea viwanda hivyo pamoja na kushiriki semina elekezi ya mafunzo ya usalama na afya iliyofanyika tarehe 10/09/2023 Mkoani Arusha huku akiiomba kamati hiyo kuitikia wito pindi ofisi yake itakapo wahitaji tena.  

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imetembelea Kwanda cha kuzalisha mbegu na mbogamboga cha Rajik Zwaan kilichopo Mkoani Arusha pamoja na kiwanda na mashamba ya Kilimanjaro Plantation Limited kilichopo Mkoani Kilimanjaro.