WAKUU WA IDARA ZA UTAWALA NA RASILIMALI WATU WAASWA KUSHIRIKIANA NA OSHA KULINDA NGUVU KAZI
Wakala wa Usalama na A fya Mahali pa Kazi (OSHA) umewataka Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimali watu kushirikiana na taasisi hiyo katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya katika maeneo yao ya kazi ili kuleta tija kwa taifa.
OSHA imetoa wito huo kupitia kwa Afisa Mafunzo wake, Bw. Simon Lwaho mara baada ya kuwasilisha mada ya masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ulioenda sambamba na zoezi la upimaji wa magonjwa yatokanayo na kazi katika Kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma kinachofanyika kwa siku tatu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).
“Kupitia kikao kazi hiki tumewaeleza Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimali watu kuwa wanapowekeza katika kulinda usalama na afya za wafanyakazi wao wanaongeza tija katika utoaji wa huduma katika maeneo yao ya kazi, taasisi ya OSHA inaendelea kuwakumbusha wakuu hawa kuhakikisha wanashirikiana nasi katika kuimarisha mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi kwasababu ni hitaji la kisheria linalotakiwa kusimamiwa kwa kuhusisha wadau wakubwa watatu ambao ni sisi OSHA kwa upande wa serikali, wao Wakuu wa Idara za Utawala pamoja na wafanyakazi ambao ni kiungo muhimu katika kuleta maendeleo ya taifa letu.” alisema Bw. Simon Lwaho.
Aidha Mkaguzi wa Afya wa OSHA, Bi Amina Nangu amesema kuwa Wakuu hawa wa Idara za Utawala ndio watoa maamuzi katika maeneo yao ya kazi hivyo wakielewa vyema Sheria na miongozo ya usalama na afya mahali pa kazi wataweza kuisimamia utekelezaji wake ipasavyo.
“OSHA tumeshiriki katika kikao kazi hiki ili kutoa elimu kadhalika kuendesha zoezi la upimaji wa magonjwa yatokanayo na kazi tukiamini kuwa wakuu hawa wa idara za utawala wakielewa vizuri umuhimu wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi basi wataweza kusimamia na kuteleleza vizuri sheria na miongozi hii kwasababu wao ndio watoa maamuzi katika maeneo yao ya kazi” alisema Bi. Amina Nangu
Kwa upande wao wakuu hao wa Idara za Utawala katika Utumishi wa Umma kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekiri kuwa ni muhimu sana watumishi kutambua hali zao za kiafya hususan kufanya uchunguzi wa magonjwa yatokanayo na kazi huku wakiahidi kuitumia vyema elimu iliyotolewa na OSHA kupitia kikao kazi hicho.
“Ni muhimu sana kwa watumishi wa umma kufanya uchunguzi wa magonjwa yatokanayo na kazi kwa sabababu hii itasaidia kutambua hali zetu za kiafya ikiwemo kubaini kama kuna madhara yoyote yaliyotokana na kazi tunazofanya pia elimu hii iliyotolewa na OSHA itatusaidia katika kuepukana na vihatarishi mbalimbali vya ajali na magonjwa katika maeneo yetu ya kazi” alisema Bi. Judith Bosco.
Nae Bw. Erick Bazompora ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala katika Manispaa ya Bukoba amesema kuwa watumishi wanapotambua hali zao za kiafya mapema ni rahisi kujikinga dhidi ya madhara husika na kwa kufanya hivyo itasaida kupunguza gharama za uendeshaji wa eneo la kazi pamoja na kuleta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla kutoka na kuwa wafanyakazi hawa wanafanyakazi katika mazingira salama na yanayolinda afya zao.
Kikao Kazi hicho cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma kinafanyika kwa siku tatu kuanzia Oktoba 11 hadi 13, 2023 na kilifunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi – Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Boniface Simbachawene kikiongozwa na kauli mbiu inayosema “Usimamizi wa Rasilimali Watu Unaozingatia Maadili, Sheria, Uwajibikaji na Matumizi ya TEHAMA ni Msingi wa Utaoaji Huduma Bora katika Sekta ya Umma.