Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

Katibu Mkuu Luhemeja awapa changamoto OSHA


 
Na Mwandishi Wetu
 
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhandisi Cyprian Luhemeja, ameutaka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kugeuza changamoto walizonazo kuwa fursa katika jitihada za kuimarisha usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.
 
Ametoa changamoto hiyo leo (Machi 14, 2024) alipokuwa akifungua Kikao cha Pili cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika Jijini Arusha.
 
Katibu Mkuu Luhemeja amesema changamoto zilizoainishwa katika taarifa ya Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, ambazo ni pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya usalama na afya miongoni mwa wadau na ongezeko la vihatarishi vipya kwenye maeneo ya kazi vinavyotokana na ukuaji wa kasi wa teknolojia zinazotumika mahali pa kazi, zinapaswa kubadilishwa kuwa fursa ambazo zinaweza kutumika kuiimarisha Taasisi ya OSHA.
 
“Changamoto mlizozieleza binafsi sizioni kama changamoto bali ni fursa ambayo kama OSHA mnaweza kuitumia kujijenga na kukua zaidi katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi,” amesema Mhandisi Luhemeja na kuongeza:
“Mnachopaswa kufanya ni kuweka mipango mizuri, kuongeza ushirikishwaji wa masuala ya Taasisi miongoni mwenu na kufanya kazi kwa juhudi na ubunifu katika kutafuta matokeo mnayoyahitaji.”
 
Akitoa maelezo ya awali kuhusu kikao hicho cha baraza la wafanyakazi, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Mwenda, amesema kikao hicho ni maalum kwa ajili ya kujadili bajeti ya mwaka wa fedha ujao (2024/2025).
 
“Katika kikao hiki bajeti na malengo yaliyoainishwa yatafanyiwa mjadala wa kina na wajumbe na hatimaye kukubaliana kuhusu utekelezaji wake kwa mustakabali mzima wa maendeleo ya Taasisi yetu ya OSHA,” ameeleza Mtendaji Mkuu.
 
Aidha, Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA ameeleza kuwa katika kutekeleza malengo yaliyopangwa likiwemo suala la kuongeza usajili wa maeneo ya kazi, wamejipanga kutumia zaidi mifumo ya TEHEMA ili kuwafikia watu wengi zaidi kwa wakati muafaka.
 
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Comrade Hery Mkunda, ambaye alikuwa Mgeni Mwalikwa katika kikao hicho, ameipongeza OSHA kwa kutekeleza sheria inayowataka waajiri kufanya mikutano ya mabaraza ya wafanyakazi kama nyezo muhimu ya ushirikishwaji ndani ya Taasisi husika.
 
“TUCTA tumekuwa tukishirikiana vizuri na OSHA katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanakuwa salama mahali pa kazi kupitia kuhamasisha waajiri kuunda Kamati za Usalama na Afya kwenye maeneo yao ya kazi. Aidha, tumekuwa tukishirikiana na OSHA kuhakikisha kwamaba wafanyakazi wanapatiwa mafunzo ya usalama na afya wakiwemo viongozi wa matawi wa vyama vya wafanyakazi,” ameeleza Comrade Mkunda.