Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

Kuelekea siku ya Usalama na Afya Duniani Serikali yawataka waajiri kusajili maeneo ya kazi OSHA

Na Mwandishi wetu

Kuelekea Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Serikali imewataka waajiri nchini kutekeleza ipasavyo matakwa ya Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ikiwemo kusajili maeneo ya kazi katika Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ili Taasisi hiyo iweze kuwafikia na kuwapa miongozo inayohitajika kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vya magonjwa na ajali mahali pa kazi.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Deogratius Ndejembi katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika katika Ofisi za OSHA jijini Dodoma.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kutoa taarifa kwa umma kuhusu maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani yanayofanyika Kitaifa Mkoani Arusha kuanzia Aprili 23 na kufikia kilele chake Aprili 28, 2024 ambapo Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dotto Biteko, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.

“Natoa rai kwa wawekezaji wote ambao bado hawajasajili maeneo yao ya kazi OSHA kuhakikisha wanafanya usajili mara moja pamoja na kuendelea kutekeleza taratibu mbalimbali za usalama na afya kwa mujibu wa Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003,” ameeleza Mheshimiwa Waziri na kuongeza:

“Mwajiri anapokaidi kusajili eneo lake la kazi anahatarisha usalama na afya za wafanyakazi wake katika eneo la kazi husika ndio maana tunawasisitiza kuwa ni muhimu sana maeneo yote ya kazi kusajiliwa na kufikishiwa huduma za ukaguzi na ushauri na wataalam wa masuala ya usalama na afya wa OSHA,” Alisema Waziri Ndejembi.

Agizo hilo la Waziri mwenye dhamana ya Masuala ya Kazi, Mhe. Ndejembi, linaendana na kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu ambayo ni; Athari za mabadiliko ya tabia nchi katika Usalama na Afya Kazini: Sajili eneo la kazi OSHA katika harakati za kupunguza athari hizo.

Aidha, Waziri Ndejembi ametoa wito kwa waajiri na wafanyakazi kote nchini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya usalama na afya mahali pa kazi yanayofanyika Kitaifa Mkoani Arusha yakihusisha shughuli mbali mbali zinazolenga kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi.

Shughuli zilizoainishwa kutekeleza kama sehemu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni pamoja na; Mafunzo kwa wajasiriamali wadogo, maonesho ya usalama na afya mahali pa kazi, bonanza la michezo kwa wafanyakazi, shindano la tuzo miongoni mwa waajiri wanaozingatia ipasavyo taratibu za usalama na afya pamoja na kuendesha kliniki ya uchunguzi wa magonjwa mbali mbali yakiwemo yasiyoambukiza, magonjwa ya akina mama pamoja magonjwa yatokanayo na kazi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema siku ya usalama na afya mahali pa kazi duniani inalenga kuhamasisha uwepo wa mazingira salama katika maeneo ya kazi ambapo OSHA imejipanga ipasavyo kuhakikisha inayafikia maeneo yote ya kazi kwa sekta zote rasmi na zisizo rasmi.

“Tunafahamu kuwa sekta isiyo rasmi inayokabiliwa na vihatarishi vingi sana hivyo basi kama sehemu ya maadhimisho, OSHA tumejipanga vizuri sana kuhakikisha tunayafikia makundi mbalimbali ya wajasiriamali ikiwemo mama ntilie, waendesha pikipiki (boda boda), wachimbaji wadogo na hata makundi ya walemev. Hii yote ni kuhakikisha masuala ya usalama na afya yanaeleweka na kuzingatiwa na watu wote katika jamii yetu,” alisema Bi. Mwenda.

Katika mkutano huo wa Vyombo vya Habari, Waziri Ndejembi aliambatana na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokya, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri (ATE), Bi. Suzanne Ndomba – Doran pamoja na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bi. Getrude Sima.