Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

OSHA NA TAPSOA WAKUBALINA KUIMARISHA USALAMA NA AFYA VITUONI

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na Chama cha Wamiliki na Waendeshaji wa Vituo vya Mafuta Nchini (TAPSOA) wamekubaliana kushirikiana katika kuboresha hali ya usalama na afya za wafanyakazi wa vituo vya mafuta nchini kupitia ukaguzi, mafunzo pamoja na ushauri utakaokuwa unatolewa na wataalam wa OSHA katika vituo hivyo.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao cha mashauriano baina ya menejimenti ya OSHA na wanachama wa TAPSOA wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kilichofanyika jijini Mwanza ambapo pande hizo mbili zilikutana kujadiliana kuhusu namna bora ya kutekeleza Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake. 

Kikao hicho kilifunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama ambaye pamoja na kusisitiza OSHA na TAPSOA kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa sheria tajwa, alielezea umuhimu wa sekta ya mafuta katika uchumi wa nchi.

“Nani anasema nyinyi hamjachangia nchi hii kufikia uchumi wa kati, kimsingi mmekuwa na mchango mkubwa katika kufika uchumi wa kati. Kama nchi tunataka kupambana na umaskini na nyinyi ni wadau muhimu ambao mtatusaidia katika hilo  kama nilivyoelezwa awali hapa kwamba asilimia 66 ya wawakezaji wa vituo vya mafuta nchini ni Watanzania na zaidi ya asilimia 60 ya wafanyakazi katika sekta hii ni wanawake hivyo mnaweza kuona jinsi sekta hii ilivyo muhimu katika uchumi na maendeleo ya Taifa letu na kwasababu hiyo ni lazima tuitunze ili nayo itutunze,” amesema Waziri Mhagama katika hotuba yake ya kufungua kikao hicho. 

Katibu Mkuu wa TAPSOA, Bw. Augustino Mmasi, ambaye alikuwa Mwenyekiti Mwenza wa kikao hicho, amesema wanachama wake wanaamini kwamba endapo hoja na mapendekezo yao yanayotolewa kupitia vikao mbalimbali vya kuelimishana, basi azma ya serikali ya kuondoa ama kudhibiti vihatarishi katika sehemu za kazi itaweza kufikiwa.  

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema chimbuko la makubaliano hayo ni tathmini iliyofanywa na Taasisi yake katika usimamizi wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ambayo ilibainisha ombwe katika ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za usalama na afya nchini ambazo ni muhimu katika uundaji wa sera za nchi zinazohusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

“Tulifanya tathmini ya namna tunavyosimamia masuala ya usalama na afya nchini na kubaini kwamba kwa utaratibu tuliokuwa nao ilikuwa ni vigumu kuyafikia maeneo mengi ya kazi, kufanya ukaguzi na kushauri namna ya kuboresha zaidi mifumo ya usalama na afya hivyo tukaja na utaratibu wa kufanya kaguzi zetu kisekta ambapo kupitia utaratibu huto tumepata mafanikio makubwa ikiwemo kuzifikia sekta zote muhimu ikiwemo sekta ya madini, mawasiliano, huduma za fedha, bandari na viwanda,” alisema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu yenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake kupitia kusajili maeneo ya kazi nchini na kuyafikia kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa usalama na afya na kushauri juu ya namna bora za kuimarisha mifumo ya Usalama na Afya mahali pa kazi.