Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

OCCUPATIONAL SAFETY AND HEALTH AUTHORITY

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

OCCUPATIONAL SAFETY AND HEALTH AUTHORITY

image

SERIKALI YATOA SIKU 90 WAMILIKI KUSAJILI MAENEO YA KAZI OSHA

Serikali imewataka wamiliki wa maeneo ya kazi nchini ambao maeneo yao hayajasajiliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kusajili maeneo hayo ndani siku tisini kuanzia Januari 2026.

Agizo hilo la serikali limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za OSHA zilizopo Kinondoni Jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo ambayo ni ya kwanza kwa Taasisi ya OSHA tangu Waziri huyo alipoteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kusimamia masuala ya kazi nchini, imelenga kujifunza jinsi OSHA pamoja na Taasisi nyingine chini ya Wizara yake zinavyotekeleza majukumu yake.

Akizungumza na menejimenti na watumishi wa OSHA leo (Desemba 22, 2025), Waziri Sangu amesema Taasisi ya OSHA inayo dhamana kubwa ya kulinda nguvukazi ya Taifa dhidi ya ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na mazingira ya kazi yasiyokuwa rafiki.

Aidha, Waziri Sangu amesema ili OSHA iweze kusimamia ipasavyo uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini maeneo hayo yanapaswa kutambulika na OSHA kupitia usajili.

Aidha, Waziri huyo amewataka watumishi wa OSHA kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuzingatia weledi katika kuwawezesha waajiri kusimika mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi huku akiwataka waajiri hao kuzingatia ushauri ambao umekuwa ukitolewa na wataalam wa OSHA.

“Usajili wa sehemu za kazi nchini ni kwa mujibu wa kifungu cha 16 na 17 cha Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambapo OSHA husajili maeneo ya kazi na kisha kuyafikia kwa ajili ya ukaguzi na ushauri wa kitaalam juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi,” ameeleza Waziri Sangu.

Akitoa maelezo kuhusu Taasisi ya OSHA kwa Waziri, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema yeye na watumishi wa OSHA wamefarijika kumpokea Waziri na ujumbe wake ambapo watakuwa tayari kupokea maelekezo yote ya serikali na kuyafanyia kazi ipasavyo.

“Kwa niaba ya watumishi wenzangu, nikuhakikishie kwamba hatutakubali kuwa sababu ya kukwamisha utendaji wenu bali tutajitahidi kutekeleza majukumu yetu ipasavyo na hivyo kuwafanya nyinyi viongozi wetu kutembea kifua mbele kutokana na utendaji wetu mzuri,” ameeleza Kiongozi Mkuu wa Taasisi ya OSHA, Bi. Mwenda.

Waziri Sangu ameambatana na Naibu wake, Rahma Kisuo pamoja na Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) yenye jukumu la kutoa na kusimamia miongozo ya usalama na afya mahali pa kazi ambapo katika kutekeleza jukumu hilo, husajili maeneo ya kazi na kuyafikia kwa ajili ya ukaguzi na ushauri wa kitaalam juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi.