Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

MSEMAJI WA SERIKALI AWATAKA WADAU KUSHIRIKIANA NA OSHA

Mkurugenzi wa Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, ametoa wito kwa waajiri na wafanyakazi kutoa ushirikiano kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ili waweze kunufaika na ushauri na miongozo ya kitaalam juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi ambayo hutolewa na Taasisi hiyo.

Ametoa wito huo alipotembelea banda la OSHA katika maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika viwanja vya Saba Saba jijini Dar es Salaam.

“Kwanza niwapongeze OSHA kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wanasimamia usalama mahali pa kazi wanayoifanya hivyo napenda kutoa wito katika eneo hili, watu wengi wakisikia OSHA wanakuwa na hofu lakini naomba tuwaone kama marafiki wa sehemu zetu za kazi kwakuwa wao ndio wanaokuja kutushauri ni vitu gani tuvizingatie tukiwa kazini ili tufanye kazi zetu na kurejea majumbani kwetu tukiwa salama,” amesema Msigwa nakuongeza: 

“Hivyo niendelee kuwapongeza OSHA najua mnafika katika maeneo mengi nasasa mnajulikana kila mahali kwasababu kazi yenu inaonekana na watu wanaanza kutambua. Niwaombe watanzania tuendelee kutoa ushirikiano ili majukumu haya yafanyike kikamilifu jambo ambalo ni muhimu sana kwani tukiwapa ushirikiano ndivyo wanavyoweza kutushauri na kutuongoza vizuri zaidi na hivyo tutapunguza sana athari zinazoweza kuwapata wafanyakazi katika maeneo yetu ya kazi.” 

Aidha, Msemaji Mkuu wa Serikali amewataka waajiri wote kushirikiana kikamilifu na OSHA katika kujenga mifumo madhubuti ya usalama na afya katika maeneo yao ya kazi ili kuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija unaokwenda sambamba na kujali afya za wafanyakazi. 

“Wakati mwingine tunaangalia sana gharama zinazotumika katika kushughulikia masuala ya usalama na afya lakini hatuangalii thamani ya kazi kubwa inayofanywa na OSHA kwenye maeneo yetu ya kazi hivyo ni lazima tutambue kwamba tukiwa na wafanyakazi wenye afya njema watazalisha zaidi na tutaokoa fedha nyingi zinazopotea katika matibabu ya wafanyakazi wanaoumia au kuugua kila mara pamoja na  zile zinazotumika kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wapya,” amesema Msigwa. 

Kwa upande wao baadhi ya waajiri na wafanyakazi waliotembelea banda la OSHA katika maonesho hayo wametoa maoni yao kuhusu huduma za OSHA. 

“Kiukweli kupitia maonesho haya OSHA wametusaidia sana kwa kutupatia elimu na huduma mbali mbali ikiwemo usajili wa maeneo ya kazi na vyeti vya kukidhi matakwa ya awali ya usalama na afya mahali pa kazi (compliance license) huduma ambazo pengine tungeweza kuzipata kwa gharama kubwa,” amesema Bright Dickson Fue ambaye ni mmiliki wa eneo la kazi.

Nae Mhandisi Mary Estomihi ambaye ni mfanyakazi amesema: “Nimepita hapa katika banda la OSHA na nimejifunza mambo mengi ikiwemo masuala ya usalama wa umeme mahali pa kazi pamoja na namna ya kufanya tathmini ya vihatarishi vya usalama na afya mahali pa kazi.”

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu yenye jukumu la kulinda afya na usalama wa wafanyakazi katika sekta zote hapa nchini. Taasisi hii husajili maeneo ya kazi, kufanya kaguzi mbali mbali za usalama na afya pamoja na kuto katika maeneo ya kazi husika.