Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

SERIKALI YAWATAKA WENYE VIWANDA KUIJALI NA KUILINDA NGUVUKAZI

Serikali imewataka wamiliki wa viwanda nchini kuijali na kuilinda nguvukazi inayotumika katika uzalishaji ili kuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Tamko hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, alipofanya ziara katika viwanda mbali mbali jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na Maafisa wa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA). 

Akizungumza katika ziara hiyo, Katambi amesema malengo ya serikali ya awamu ya sita ni kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia uzalishaji viwandani ambapo serikali inawajibika kujenga mazingira bora ya biashara na uwekezaji.

“Sisi kama serikali tunajitahidi kuhakikisha kwamba kunakuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli zote za uwekezaji zinazingatia sheria za nchi ikiwemo sheria za Ajira na Mahusiano Kazini, Usalama na Afya Mahali pa Kazi na hifadhi kwa jamii,” amesema Naibu Waziri na kuongeza:

“Katika ziara hii ya leo tumefanya ukaguzi wa kushtukiza katika viwanda vitano vinavyozalisha bidhaa mbali mbali zikiwemo bidhaa za plastiki ambapo tumebaini mapungufu mengi katika viwanda husika ikiwemo mazingira ya kazi yasiyo rafiki kwa wafanyakazi na uwepo vitendo vya unyanyasi kwa wafanyakazi. Hivyo, nitoe rai kwa waajiri wote nchini kuhakikisha kwamba wanatoa ajiri zenye staha ili kuendana na sheria za nchi pamoja na miktaba ya kimataifa ambayo nchi yetu imeiridhia.”

Aidha, Katambi amewakaribisha wawekezaji wenye changamoto mbali mbali katika shughuli zao kuziwalisisha changamoto hizo serikalini ili ziweze kupatiwa ufumbuzi na hivyo kuondokana na vikwazo katika uzalishaji.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kanda ya Pwani wa OSHA, Bw. George Chali, ameainisha changamoto za usalama na afya zilizobainika katika ziara hiyo zikiwemo ukosefu wa vifaa kinga miongoni mwa wafanyakazi, uwepo wa nafasi finyu za kufanyia kazi, wafanyakazi kutekeleza majukumu yao katika mtindo usiofaa kiusalama na afya (ergonomic issues).

Masuala mengine ni mifumo ya umeme isiyozingatia usalama, zana na mitambo ya kazi isiyozingatia kanuni za usalama, viwango duni vya mwanga katika maeneo ya kufanyia kazi, viwango vya juu vya kelele za mashine pamoja na ukosefu au uwepo wa huduma duni za kijamii mathalani vyoo, vyumba vya kubalishia mavazi, sehemu za kulia chakula pamoja na ukosefu wa maji safi na salama ya kunywa katika sehemu za kazi.

Kutokana na mapungufu yaliyobainika, Naibu Waziri ameziagiza Taasisi zinazohusika na changamoto hizo zikiwemo OSHA, NSSF, WCF na Idara ya Kazi kuviandikia viwanda vilivyotembelewa maboresha yanayohitajika na kufuatilia kwa karibu kuhakikisha kwamba yanafanyika kwa haraka.

Ziara hizo ambazo ni endelevu zinafanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu katika maeneo mbali mbali ya kazi nchini lengo likiwa ni kufuatilia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini pamoja na Sheria za Hifadhi kwa Jamii.