Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

WAZIRI ATOA WIKI MBILI KIWANDA KUBORESHA MAZINGIRA YA KAZI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amefanya ziara katika maeneo ya kazi Kigamboni jijini Dar es Salaam ikiwemo kiwanda cha Tanzania Ruidar Co. Ltd ambapo ametoa wiki mbili kwa uongozi wa kiwanda hicho kuboresha mazingira ya kazi ambayo yameonekana kuhatarisha afya na usalama wa wafanyakazi.

Maagizo hayo yametolewa kufuatia makubaliano baina ya uongozi wa kiwanda na Waziri akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almasi Nyangasa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda na watendaji wengine wa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. 

“Mwenye kiwanda asitishe kwanza shughuli hasa kwenye maeneo yale yanayozalisha maji machafu na maeneo mengine ambayo tumekuta yana mpangilio mbaya wa malighafi na vifaa vya kufanyia kazi ili aweke mazingira vizuri. Tumekubaliana nae kufanya hivyo na ahakikishe kwamba katika kipindi hicho anachofanya maboresho wafanyakazi wanashiriki shughuli hiyo na awalipe stahiki zao kama kawaida,” amesema Waziri Ndalichako na kuongeza:

“Tunawapenda sana wawekezaji wetu kwakuwa wanatusaidia kutengeneza ajira za Watanzania lakini tunawaomba wajitahidi kuzingatia sheria za nchi ikiwemo kuweka mazingira ya uzalishaji katika hali nzuri ili kuwaepusha wafanyakazi na magonjwa na ajali zinazoweza kusababishwa na mazingira ya kazi yasiyokuwa rafiki.”

Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almasi Nyangasa, amesisitiza kuwa kazi hiyo ya maboresho ifanyike kwa kuwatumia wafanyakazi wa kiwanda hicho na kusimamiwa na watendaji wa Ofisi yake pamoja na wale wanaotoka katika Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amewataka wenye viwanda kuwajali wafanyakazi ambao ndio msingi mkubwa wa uzalishaji kwa kuwapa vifaa kinga stahiki pamoja na mahitaji mengine ya muhimu.

“Katika ukaguzi wetu tumebaini kwamba baadhi tu ya wafanyakazi ndio wanaopatiwa vifaa kinga na wengine hawapewi. Aidha, wafanyakazi hawapatiwi maji safi na salama ya kunywa kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi jambo ambalo ni muhimu sana hususan kwa wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye maeneo yenye joto kali. Hata hivyo pamoja na kwamba suala hili lipo kisheria lakini ni jambo la kiutu,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA katika kikao cha pamoja baada ya ukaguzi katika kampuni ya Lake Oil Group.


Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda hicho, Zhang Ping, ameahidi kufanya maboresho yaliyopendekezwa na wataalam ndani ya muda uliokubaliwa na pande zote mbili.

Aidha, ujumbe huo wa Waziri mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi umetembelea Kampuni ya Lake Oil Group na kufanya ukaguzi wa mazingira ya kazi pamoja na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni hiyo. Ziara hii ni sehemu ya ziara ambazo Waziri huyo amekuwa akizifanya katika mikoa mbali mbali kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa Sheria za Kazi yakiwemo Masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi, Hifadhi kwa Jamii na Mahusiano Kazini.

Kiwanda cha Tanzania Ruidar Co. Ltd kinazalisha bidhaa mbali mbali za plastiki yakiwemo mabomba ya maji na vyombo vya majumbani.