Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

WAZIRI NDALICHAKO AWAPONGEZA WAWEKEZAJI KWA KUTOA AJIRA KWA WATANZANIA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amewapongeza wamiliki wa viwanda wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kwa kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania kupitia uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi. 

Ametoa pongezi hizo alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku mbili (2) katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambapo ametembelea viwanda na maeneo ya kazi sita (6) yanayozalisha bidhaa mbali mbali vikiwemo vifungashio, vyombo vya majumbani, mabomba, vinywaji, taulo za kike na nyama.

Maeneo yaliyotembelewa na Waziri Ndalichako ni pamoja na Lake Oil Group, Tanzania Ruidar Co. Ltd vya Kigamboni pamoja na Tanchoice Limited, U-fresh Food Limited, Keds Tanzania Ltd na Global Packaging Limited.

Katika ziara hiyo, Waziri Ndalichako ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya (OSHA), Khadija Mwenda, Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa, watendaji wengine wa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Wilaya za Kigamboni na Kibaha.

 “Nimehitimisha ziara yangu ya siku mbili katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Lengo la ziara hii ilikuwa ni kupata mrejesho wa utekelezaji wa Sheria za Kazi ikiwemo kuangalia ajira zinazozalishwa na wawekezaji wetu. Jambo la kufurahisha ni kwamba katika maeneo yote sita niliyotembelea nimeona zaidi ya ajira 3,000 zimezalishwa,” amesema Prof. Ndalichako.

Aidha, amesema wengi wao kati ya idadi hiyo yote ni vijana jambo ambalo linadhihirisha kwamba serikali ya awamu tano inatekeleza ipasavyo wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini.

Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo kwa wawekezaji, Prof. Ndalichako amebainisha kwamba kumekuwa na dosari ndogo ndogo katika maeneo ya kazi aliyoyatembelea ikiwemo baadhi ya waajiri kutotoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, kutowasilisha michango katika mifuko ya hifadhi kwa jamii pamoja na baadhi ya maeneo kutokuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.

Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri, amemshukuru Waziri Ndalichako kwa kufanya ziara katika Wilaya ya Kibaha na kuwakumbusha waajiri kuzingatia Sheria za Kazi ambapo ameahidi kushirikiana na wawekezaji katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri. 

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amewataka wawekezaji kushirikiana kwa karibu na Ofisi yake katika kuboresha mazingira ya kazi.

“Wakati wote sisi tupo tayari kushirikiana nanyi kutengeneza mifumo ya usalama na afya kwenye maeneo yenu ya kazi ili ajira hizi mnazozizalisha kwa wingi ziwe endelevu na zilete tija kwenu, kwa wafanyakazi wenyewe na Taifa kwa ujumla,” amesema Mkaguzi Mkuu wa maeneo ya kazi nchini.