Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

OSHA yatoa mafunzo ya Usalama na Afya kazini kwa Wahariri

Na Mwandishi Wetu

Wito umetolewa kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini kutumia nafasi zao kuwaelimisha waajiri na wafanyakazi kuhusiana na uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika sehemu za kazi ili kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyoweza kusababishwa na vihatarishi vya usalama na afya mahali pa kazi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, alipofungua semina kuhusu usalama na afya kazini iliyoandaliwa na OSHA na kutolewa kwa wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari nchini. 

DC Mtambule amesema kutokana na jitihada zinachukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita kuhamasisha uwekezaji nchini shughuli za nyingi za kiuchumi zimekuwa zikianzishwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi jambo linalohitaji wahusika katika uzalishaji kuwa na uelewa wa kutosha wa masuala ya afya na usalama kazini.

“Uchumi wa nchi yetu unakuwa kwa kasi na uwekezaji unaongezeka kila siku. Mathalani Wilaya ya Kinondoni pekee kwasasa ina zaidi ya viwanda 150 ukiachilia mbali shughuli nyingine za kiuchumi zinazoajiri mamilioni ya Watanzania. Hivyo, unaweza kuona ni kwa jinsi gani kuna umuhimu wa kuhakikisha sehemu za kazi zinakuwa na mifumo imara ya kulinda nguvukazi pamoja kuhakikisha kwamba waajiri na wafanyakazi wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya taratibu muhimu za usalama na afya mahali pa kazi,” ameeleza Mtambule na kuongeza:

“Ili kufanikisha jukumu hilo la kuelimisha jamii ya waajiri na wafanyakazi, OSHA inawahitaji wahariri kama wadau muhimu ambao mnaweza kufikisha elimu hiyo kwa haraka zaidi na ndio maana wameona ni vema mkapatiwa mafunzo haya. Hivyo, niwapongeze kwa kazi kubwa mnayofanya lakini ninawaomba muendelee kushirikiana na OSHA na Serikali kwa ujumla katika kuhabarisha na kuwaelimisha Watanzania kuhusiana na masuala mbali mbali likiwemo suala usalama na afya kazini.”

Aidha, DC Mtambule ameipongeza OSHA kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake na amewataka watendaji wa Taasisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuwachukulia hatua waajiri wote wanavunja sheria ya usalama na afya kazini.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amewashukuru wahariri kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiutoa kwa Taasisi ya OSHA katika kutekeleza majukumu yake ya msingi.

Aidha, ameeleza malengo ya semina hiyo kuwa ni kuwajengea wahariri hao uelewa kuhusiana na Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi pamoja na taratibu mbali mbali zinazosimamiwa na OSHA katika maeneo ya kazi nchini ili kuwaweka katika nafasi nzuri ya kutoa elimu kwa umma.