Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

WADAU NCHINI WAVUTIWA NA TUZO ZA USALAMA NA AFYA KAZINI

Tuzo za Usalama na Afya Mahali pa Kazi maarufu kama AOSH zimeendelea kuwa na mvuto miongoni mwa wadau wa usalama na afya mahali pa kazi nchini ambapo kwa mwaka 2026 idadai ya washiriki imeongezeka maradufu hadi kufikia washiriki zaidi ya 500 kutoka 20 tuzo hizo zilipoanzishwa mwaka 2004.

Tuzo hizi huandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) kwa kushirikiana na wadau wa utatu katika usimamizi wa masuala ya Usalama na Afya ambao ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wakishauriwa kwa karibu na Shirika la Kazi Duniani (ILO) hususan katika eneo la viwango vya Kimataifa.

Kwa mwaka huu (2026) hafla ya kukabidhi tuzo hizo kwa washindi imefanyika Mkoani Njombe ikihiitimisha Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi iliyohusisha shughuli mbalimbali za uhamasishaji uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

Akihutibia mamia ya wadau walioshiriki hafla hiyo usiku wa Aprili 29, 2026, Mgeni Rasmi ambaye ni Waziri Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu amesema kuwa Tuzo za Usalama na Afya Mahali pa Kazi (AOSH), zimekuwa kichocheo kikubwa cha uzingatiaji wa sheria na kanuni za usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.

Waziri Sangu ameeleza kuwa tuzo hizo zimekuwa na mchango chanya katika kuhamasisha waajiri na wafanyakazi kuboresha mazingira ya kazi na hatimaye kuzalisha kwa tija.

Ameongeza kuwa ushindani wa tuzo hizo umekuwa ukiwahamasisha waajiri kuongeza ubunifu na kufanya maboresho ya mara kwa mara katika mifumo ya kuzuia ajali na magonjwa na hivyo kupunguza vifo na majeraha kwa wafanyakazi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda ameainisha malengo ya tuzo hizo kuwa ni pamoja na; kuhamasisha uzingatiaji wa sheria, kanuni, miongozo na viwango bora vya usalama na afya mahali pa kazi, kuimarisha utamaduni wa kujali na kuzingatia masuala ya usalama na afya kazini pamoja na kutambua ubora na jitihada zinazofanywa na wadau katika kuimarisha afya na usalama wa wafanyakazi.

Aidha, amesema tuzo hizo ni sehemu ya kampeni pana ya OSHA inayolenga kuijengea jamii utamaduni wa kuzingatia masuala ya usalama mahali pa kazi ambaye imekuwa ikifanyika sambamba na shughuli nyingine yakiwemo maonesho ya usalama na afya mahali pa kazi, mafunzo na uwezeshaji wajasirimali wadogo katika kuadhimisha siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ambayo hufanyika Aprili 28 kila mwaka.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waaajiri Tanzania (ATE), Bi. Suzanne Ndomba-Dorani, alitoa ufafanuzi kuhusu mchakato wa tuzo hizo akitanabaisha kwamba miongoni mwa vigezo muhimu vilivyotumika kupata washindi wa tuzo za mwaka huu viliwekwa katika makundi mawili.

Kundi la kwanza la vigezo hivyo ni pamoja na; maeneo ya kazi yaliyosajiliwa na OSHA, yaliyoonesha nia ya kushiriki kupitia utaratibu uliowekwa na yaliyofanyiwa tathmini ya umahiri katika uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya kwa mujibu wa vigezo vya Kitaifa na Kimataifa ambavyo hotelewa na Shirika la Kazi Duniani (ILO)” ameleza Mkurugenzi wa ATE na kuongeza:

Kundi la pili linahusisha vigezo kama vile; Ushiriki wa kampuni katika shughuli mbalimbali za maadhimisho na jinsi kampuni husika ilivyojipanga kushiriki pamoja na mapitio ya taarifa zinazoonesha jitihada za kampuni au watu binafsi katika kuhamasisha masuala ya usalama na afya kazini pamoja na mchango wake katika kuwezesha shughuli za usimamizi wa Sheria ya Usalama na Afya kazini ndani ya kipindi cha mwaka mmoja”. 

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeng’ara kwa kuibuka mshindi wa jumla katika tuzo za mwaka huu ambapo pia imejinyakulia tuzo nyingine 11 katika vipengele mbalimbali.

Tuzo za mwaka huu yaani AOSH 2026 ni za 21 tangu zilipoanza kutolewa mwaka 2004 na mwaka huu washindi wa tuzo hizo wamepatikana kutoka makundi (categories) 30 ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.