Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

OSHA YAGUSA MAISHA YA WAKAZI WA MKOA WA KILIMANJARO

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umegusa maisha ya wananachi wa Mkoa wa Kilimanjaro kupitia kampeni yake ya huduma kwa jamii ambapo imekabidhi vifaa vya msaada katika mashule, hospitali pamoja na kutoa mafunzo ya usalama na afya kwa wajasiriamali wadogo zaidi ya 500.
 
 Makundi yaliyonufaika na kampeni hiyo ni kutoka Wilaya za Mwanga na Moshi Mjini ambapo OSHA imepanda miti 200 ya matunda katika shule mbalimbali za msingi na sekondari ndani ya Wilaya ya Mwanga.
 
 Aidha, imekabidhi mashuka 100 katika Hospitali ya Wilaya ya Mwanga, vifaa vya michezo pamoja na kutoa mafunzo ya usalama na afya yaliyofanyika sambamba na kukabidhi vifaa kinga kwa makundi ya wajasiriamali wadogo wenye ulemavu pamoja na maafisa usafirishaji (bodaboda).
 
 Akizungumza katika kilele cha kampeni hiyo katika Viwanja vya Chuo cha Polisi Moshi, Mgeni Rasmi wa Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR Bonanza 2026) ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, amesema lengo la kampeni hiyo ni kugusa maisha ya makundi yenye mahitaji maalum katika jamii.
 
 “Miongoni mwa makundi yaliyonufaika na kampeni hii ni pamoja na Maafisa Usafirishaji (Bodaboda) 200 wa Wilaya ya Mwanga na Moshi, Wanachama 70 kutoka Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Shule za msingi na sekondari Mwanga pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Mwanga,” ameeleza Mheshimiwa Timbuka.
 
 Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema tukio hilo ni utekelezaji wa mkakati wa OSHA wa kurudisha kwa jamii sambamba na utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya kusimamia uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.
 
 Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mwanga Mpampalika Mfaume pamoja na wanufaika wa kampeni hiyo, wameishukuru Taasisi ya OSHA kwa kubana matumizi yake ili kuwezesha upatikanaji wa mahitaji ya msingi kwa makundi mbalimbali ya jamii.
 
 “Nimefurahia mafunzo ya leo kwasababu nimefahamu kazi za OSHA na zaidi nimejifunza kwamba usalama si tu kwa wafanyakazi walioajiriwa bali hata kwetu sisi tuliojiajiri tunatakiwa kuzingatia misingi ya usalama na afya kazini,” Bi. Judika Allen Mshiriki wa Mafunzo.