Occupational Safety and Health Authority
  +255-22-2760548 / 2760552       info@osha.go.tz                     

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI

image

Namna Tanzania ilivyoadhimisha siku ya usalama na afya duniani

Aprili 28 kila mwaka ni siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ambapo jana Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani katika kuadhimisha siku hiyo.

Maadhimisho hayo mwaka huu yamefanyika kitaifa jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako.

Kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu ni: Kwa Pamoja tushirikiane kujenga utamaduni bora wa Usalama na Afya mahali pa kazi (Act together to build a positive safety and health culture). 
 
Akitoa taarifa ya maadhimisho ya mwaka huu katika siku ya kilele cha maadhimisho (Aprili 28, 2022), amesema lengo la maadhimisho hayo nikuendeleza kampeni za kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za watu katika sehemu za kazi.

Aidha, alieleza kuwakampeni ya mwaka huu imejikita zaidi katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na ushirikishwaji katika ngazi zote za maamuzi wakiwemo wafanyakazi ili nao wawe sehemu ya maamuzi na hivyo kujenga utamaduni wa kukinga zaidi kuliko kusubiri mambo yaharibike ndipo hatua za kuyarekebisha zichukuliwe. 

“Utamaduni huu ukijengeka utapelekea kupunguza ajali, magojwa na vifo vinavyotokana na mazingira hatarishi ya kazi na hivyo kuongeza tija katika uzalishaji ndani ya Taifa letu,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA, miongoni mwa shughuli zinazotekelezwa katika kampeni ya uhamasishaji ya mwaka huu pamoja na; Mafunzo ya Usalama na Afya kwa wajasiriamali wadogo katika sekta mbali mbali wakiwemo wachimbaji wadogo, wazalishaji wa mazao ya misitu, wenye viwanda vidogo chini ya SIDO, watu wenye ulemavu pamoja na wanafunzi wa vyuo vya ufundi stadi na elimu ya juu.

Shughuli nyingine ni maonesho ya usalama na afya mahali pa kazi, shindano la tuzo za usalama na afya mahali pa kazi miongoni mwa maeneo mbali mbali ya kazi pamoja na ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya katika ofisi za Wizara na Ofisi mbali mbali za serikali.

Akihutubia mamia ya wakazi wa Dodoma na washiriki wa shughuli za maadhimisho kutoka katika mikoa mbali mbali nchini, Waziri Ndalichako ametoa wito kwa wadau wote wa masuala ya usalama na afya (Serikali, Waajiri na Wafanyakazi) kushirikiana katika kujenga utamaduni wa kuzuia vihatarishi vya usalama na afya kwa kuweka mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.

“Kwa ujumla ukiwauliza wafanyakazi sababu ya ajali kutokea, wengi wao watajibu ajali ni matokeo ya mazingira mabaya ya kazi na ukiwauliza waajiri wao watajibu kuwa ajali husababishwa na uzembe wa wafanyakazi. Hivyo, tunapoadhimisha siku hii leo, ni vema kuwahimiza wadau wote wawe na mjadala mpana wa namna ya kuimarisha utamaduni wa kuzuia vihatarishi miongoni mwa jamii yetu,” amesema Prof. Ndalichako.

Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani chimbuko lake ni iliyokuwa siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka waliopoteza maisha na kuumia kazini. Siku hiyo ya kuwakumbuka waathirika hao ilianza kuadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1996 huko Marekani katika jiji la Newyork. 

Kwa hapa nchini, siku hii ambayo maadhimisho yake huratibiwa na serikali kupitia Taasisi ya OSHA yalianza kuadhimishwa mwaka 2004 ambapo kwa mwaka huu maadhimisho haya yanafanyika kwa mara ya 18.