WAZIRI SANGU: KAGUZI ZA OSHA ZACHOCHEA MABORESHO SEKTA YA MADINI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, amesema kaguzi zinazofanywa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) zimechangia maboresho makubwa katika sekta ya madini nchini.
Amesema hayo baada ya kutembelea Maonesho ya Sekta ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bomba Mbili, mjini Geita.
Waziri Sangu amesema maboresho hayo yana umuhimu mkubwa katika kuimarisha usalama na afya mahali pa kazi, huku sekta ya madini ikiendelea kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Ameongeza kuwa maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika kila mwaka mwezi Aprili yamekuwa yakichochea mwamko wa wadau wa sekta ya madini kushiriki katika juhudi za kuboresha usalama na afya mahali pa kazi, kutokana na elimu wanayoipata.
Aidha, Waziri huyo ameipongeza OSHA kwa kuendesha mafunzo kwa wajasiriamali kupitia kampeni zinazolenga kuwafikia wadau wengi zaidi na kuwajengea uwezo wa kuzingatia masuala ya usalama na afya katika shughuli zao.
“Tumetoka OSHA ya udhibiti, tumekuwa na OSHA mpya yenye mwelekeo wa kuwezesha wafanyabiashara na sekta mbalimbali kujikita zaidi katika uzalishaji kuliko kuiona taasisi kama chombo cha udhibiti,” alisema Sangu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema ushiriki wa taasisi hiyo katika maonesho hayo unalenga kutoa elimu kuhusu usalama na afya mahali pa kazi, kurasimisha usajili wa maeneo ya kazi na kutoa huduma za upimaji wa afya.
Mwenda amesema maeneo ya migodi yana vihatarishi mbalimbali vinavyoweza kuathiri usalama na afya za wafanyakazi, hivyo OSHA imeona umuhimu wa kushiriki katika maonesho hayo ili kuwafikia wadau, kutoa elimu na kusogeza huduma karibu na wananchi.